WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, sasa yuko katika hatari ya kuondolewa madarakani
kwa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye kufuatia tuhuma nzito za ubadhirifu
wa fedha za umma unaodaiwa kuwahusisha mawaziri watano wakiongozwa na Waziri wa
Fedha Mustafa Mkulo.
Akiwasilisha majumuisho ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma,
mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe, aliliambia Bunge kuwa kuanzia leo
wataanza kukusanya saini za wabunge wenye nia ya kupiga kura hiyo na kwamba
uamuzi wake utawasilishwa bungeni Jumatatu wiki ijayo.
Mwenyekiti huyo alisema ikiwa mawaziri hao ambao hata hivyo hakuwataja majina
mmoja baada ya mwingine hawatakuwa wamejiuzulu wenyewe hadi kufikia siku hiyo,
basi wabunge watamwondoa Pinda madarakani kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani
naye.
Kwa hali hiyo, Zitto alisema kuwa itakuwa ni jukumu la mawaziri hao kabla ya
Jumatatu wiki ijayo kuamua wenyewe kujiuzulu au kumwacha waziri mkuu
atimuliwe.
Hatua hiyo ya Zitto ilitokana na hoja iliyokuwa imetolewa mapema na Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), ambaye aliwataka wenyeviti wa kamati
za Bunge wakati watakapokuwa wanajumuisha hoja zao kupendekeza kupiga kura ya
kutokuwa na imani na waziri mkuu Pinda ikiwa mawaziri wake hawatakuwa
wamejiuzulu wenyewe.
Lissu alisema wakati wa kupiga kelele umekwisha, na sasa wanachotakiwa ni
kuchukua hatua, kwani mamlaka hiyo wanayo kwa mujibu wa Katiba.
“Waziri Mkuu wajibika kwa madudu ya serikali. Nitaomba wenyeviti wa kamati
hizi wanapomalizia mjadala huu kupendekeza kura ya kutokuwa na imani na waziri
mkuu kwa kujenga mfumo wa siasa wa udokozi. Tukifanya hivyo wananchi
watatuamini. Ninyi chama tawala ndio mnaosababisha haya kama mtatumia wingi wenu
sawasawa tutafanikiwa, sisi tupo wachache.
“Badala ya kupiga makofi, chukua hatua kwa uozo huu. Mkifanya hivyo
mtaheshimika na msipofanya hivyo mtaingia kwenye vitabu vya historia,”
alisema.
Alisema masuala ya ufisadi yamekuwa yakizungumzwa na zaidi ya miaka 10 sasa,
lakini hawajawahi kuona serikali ikichukua hatua.
“Wakati kila mwaka CAG anatuletea taarifa za wizi, hatujawahi kuona serikali
ikichukua hatua dhidi ya wahusika. Hatujawahi kuona mtendaji amechukuliwa hatua
wala waziri kuwajibika katika hili. Watu wanapata kupata nafasi za uwaziri ili
kuhujumu nchi,” alisema na kuongeza mfumo uliopo ni wa kulinda wezi.
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=35063
No comments:
Post a Comment